Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
JESHI la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kamandi ya Anga, itafanya maadhimisho ya
miaka 32 tangu kuanzishwa kwake kwa kuonesha zana za kivita
zilizonunuliwa na Serikali kwa ajili ya ulinzi imara.
Akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Anga
nchini, Meja Jenerali Joseph Kapwani, alisema maonesho hayo yatafanyika
jijini Mwanza ili kutoa fursa kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa,
kujionea zana za kisasa.
Alisema maadhimisho
hayo yatakuwa ya kwanza kufanyika nchini tangu kuanzishwa kwa Kamandi ya
Anga mwaka 1982 na yatafanyika kuanzia Julai 23 mwaka huu na kilele
chake Julai 28 mwaka huu.
"Lengo la maadhimisho
haya kwanza ni kusherehekea umri wa miaka 32 kwa kujitathmini kiutendaji
ndani ya Kamandi, pili ni kutoa fursa kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa
kuziona zana mbalimbali zilizonunuliwa na Serikali," alisema.
Alisema pamoja na
jukumu la Kamandi hiyo kuhakikisha anga ya Tanzania inakuwa salama
wakati wote, pia wana majukumu mengine ya ziada ambayo ni pamoja na
kutoa msaada wa kimapigano kwa wanajeshi wa nchi kavu na yale ya majini.
Majukumu mengine ni
kuzisaidia mamlaka za kiraia wakati wa maafa ya kitaifa, kusindikiza
ndege za viongozi, kukusanya taarifa za kiusalama, kushiriki katika
operesheni za kulinda amani za Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Mataifa
(UN) na kuendeleza uhusiano wa kijeshi na nchi zingine kwa njia ya
mazoezi ya pamoja.
"Kamandi hii ni
miongoni mwa Kamandi tatu zinazounda JWTZ, zingine ni Kamandi ya Jeshi
la Nchi kavu na Wanamaji na kila moja ina majukumu yake, kazi ya Kamandi
yetu ni kulinda anga.
"Jukumu hili
linatekelezwa kwa kutumia zana mbalimbali ambazo ni pamoja na ndege za
kivita, usafirishaji, makombora, mizinga ya masafa marefu na mafupi ya
kudungulia ndege na zana za upelelezi wa anga...katika maadhimisho haya,
zana zote zitakuwepo na nyingine nyingi," alisema.
Meja Jenerali Kapwani
alisema katika maonesho hayo, wananchi watapata fursa ya kuwaona
marubani watatu wa ndege za kivita ambao idadi yao imeongezeka kutoka
rubani mmoja.
Marubani hao
wataendesha ndege za usafirishaji wa anga, upelelezi na kivita ambao kwa
sasa wapo katika mazoezi kwenye nchi za China na Afrika Kusini wakiwa
na elimu nzuri.
Akizungumzia mabaki ya
ndege zilizoko Ukonga Dar es Salaam, Mwanza na zile za vita ya Kagera,
alisema ndege hizo zitatengenezwa ili ziweze kutumika na nyingine
zitabaki kama ukumbusho
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment