Home » » KATIBA MPYA NA MWAROBAINI WA UFISADI

KATIBA MPYA NA MWAROBAINI WA UFISADI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Kwa miaka 50 sasa, taifa letu limeshuhudia ufisadi wa kutisha, huku baadhi ya viongozi wakijilimbikizia mali kwa upande mmoja na Watanzania wakiendelea kuishi katika lindi la umaskini kwa upande mwingine.
Hivi sasa tunashuhudia kiongozi wa umma anapewa ofisi, lakini ndani ya kipindi kifupi anakuwa na utajiri wa kutisha, watoto wao wanakuwa na utajiri wa kutisha bila kuainisha vyanzo vyao vya mapato.
Lakini ibara 10 za Rasimu ya Pili ya Katiba zilizopendekezwa na wananchi kama zitapita zilivyo, zitakuwa ndio mwarobaini wa ufisadi kwa viongozi wa umma.
Pamoja na umuhimu wa ibara hizi kwa mustakabali wa nchi yetu, bado Watanzania hawajazipa umuhimu unaostahili na badala yake mjadala umejikita zaidi katika muundo wa muungano.
Ibara hizo 10 ambazo kwa hakika zitaongeza uwajibikaji zipo katika sura ya tatu ya Rasimu ya Pili ya Katiba zikihusu Maadili na Miiko ya uongozi na utumishi wa umma, zimeanzia ibara ya 13 hadi ya 22.
Kwa mujibu wa ibara ya 13, madaraka atakayopewa kiongozi wa umma ni dhamana na atatumia madaraka hayo kutekeleza wajibu wake kwa kuheshimu wananchi na atateuliwa kwa misingi ya haki.
Kwamba kiongozi wa umma atazingatia uwezo, pasipo upendeleo katika kufanya uamuzi na kuhakikisha uamuzi wake haufuati udugu, ukabila, udini, upendeleo, rushwa na ubaguzi.
Sote ni mashahidi namna watoto wa vigogo walivyoajiriwa katika taasisi nyeti, huku usaili wao ukidaiwa kugubikwa na upendeleo. Baadhi ya ofisi zimejaa watumishi kutoka eneo moja.
Ibara ya 14 ya Rasimu ya Katiba inambana kiongozi wa umma kwamba anapokuwa katika kazi za ofisi au binafsi atahakikisha haruhusu kutokea kwa mgongano wa masilahi kati ya binafsi na ya umma.
Mbali na ibara hiyo, ibara ya 16 inambana kiongozi wa umma kutofungua au kumiliki akaunti nje ya nchi isipokuwa kwa namba ambayo sheria za nchi zinaruhusu.
Sharti hili ni muhimu hasa ikizingatiwa kuwa zaidi ya Sh2 trilioni zinatoroshwa kila mwaka kwenda nje ya nchi, huku viongozi wa umma na vigogo wengine wakimiliki akaunti za kigeni nje.
Mbali na utoroshwaji huo wa fedha, kuna mabilioni ya Dola za Marekani, yanadaiwa kuhifadhiwa nchini Uswisi licha ya sheria kutaka wapate kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Ibara ya 16(b) inasema kiongozi wa umma “Hataomba au kupokea mkopo au faida yeyote kwa namna au mazingira ambayo yanashusha hadhi au heshima ya utumishi wa umma.
Ibara ya 17 ambayo ni muhimu mno kwa mazingira tuliyonayo sasa ya viongozi wa umma kujilimbikizia mali. Inamtaka kiongozi kutangaza mali zake anapoingia na kuacha uongozi wa umma.
“Kiongozi wa umma atalazimika kutangaza na kuwasilisha mali zake, ndani ya siku 30 baada ya kupata uongozi na baada ya kuacha uongozi, mali na thamani yake na madeni yake Tume ya Maadili,” inasomeka.
Ibara hiyo fasili ndogo ya 2 (1) inambana kiongozi wa umma kutangaza mali na madeni yake binafsi, ya mweza wake na ya watoto wake waliochini ya umri wa miaka 18 mara moja kila mwaka. Ibara ya 18, imeweka wazi kuwa kiongozi wa umma hatashiriki katika kufanya uamuzi wa jambo au shughuli yoyote ambayo ana masilahi nayo yeye binafsi, mwenza wake, watoto wake ama jamaa zake.
Hali ilivyo sasa katika nchi yetu inatisha. Baadhi ya mawaziri wanafanya biashara na Serikali, wabunge wanafanya biashara na Serikali, madiwani wanafanya biashara na Halmashauri.
Huu ni mgongano mkubwa wa masilahi. Ni mgongano mkubwa kwa sababu wabunge ndio wanaopaswa kuisimamia Serikali. Wataisimamiaje wakati inawapa mkate?
Vivyohivyo kwa madiwani, wapo baadhi sio wote, wamesajili kampuni hasa za ukandarasi ambazo zimesimama kidete na kuhakikisha halmashauri wanazozisimamia, zinazipa zabuni.
Ibara ya 21, imeweka bayana kuwa kiongozi wa umma atapaswa kuheshimu na kutii maadili ya viongozi wa umma ikiwamo miiko ya uongozi ambayo ni pamoja na kutotoa au kupokea rushwa.
Miiko hiyo ya uongozi ni pamoja na kutojilimbikizia mali kinyume cha sheria kama ambavyo nimetangulia kusema hapo juu kuwa “Utajiri wa viongozi wetu una maswali mengi kuliko majibu”. Ibara hiyo ya 21 fasili ndogo ya 2(a) (vi), inamzuia kabisa kiongozi wa umma kutumia wadhifa, nafasi au cheo chake kwa manufaa yake binafsi, familia yake, ndugu, jamaa na marafiki zake.
Kiongozi wa umma kulingana na ibara hiyo ya 21 ambaye atatuhumiwa kwa makosa ya kimaadili, udhalilishaji wa mtu au wizi au ubadhirifu wa mali za umma atakuwa amevunja katiba ya nchi.
Ibara hiyo imeweka wazi kuwa kiongozi wa aina hiyo atasimamishwa kazi hadi suala lake litakapoamuliwa kwa mujibu wa sheria za nchi au taratibu zinazohusu viongozi wa umma.
Sharti hilo ni muhimu sana, kwani kwa miaka mingi tumeshuhudia viongozi wakishitakiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi na bado wakaendelea kuhudumia wananchi. Mifano hii ipo.

Ibara ya 22 inawazuia watumishi wa umma kugombea, kuchaguliwa au kuteuliwa kushika nafasi ya madaraka katika chama cha siasa au nafasi ya madaraka ya kisiasa ya aina yoyote chini ya katiba hii.
“Mtumishi huyo atachukuliwa kuwa utumishi wake umekoma tangu siku ya kuteuliwa kuwa mgombea, kuchaguliwa au kuteuliwa kushika nafasi ya madaraka ya kisiasa au katika chama cha siasa.
Kuwapo kwa ibara hii kutasaidia kutatua kero ya muda mrefu ya viongozi wetu kuwa na kofia mbili. Ni Rais wa nchi na hapo hapo ni mwenyekiti wa taifa wa chama cha siasa. Hii haikubaliki.
 Chanzo:Mwananchi
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Rukwa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa