Home » » MKUU WA MKOA WA RUKWA INJINIA STELLA MANYANYA AKABIDHI MSAADA WA BOTI KUSAIDIA MAMA WAJAWAZITO NA WAGONJWA MWAMBAO WA ZIWA RUKWA

MKUU WA MKOA WA RUKWA INJINIA STELLA MANYANYA AKABIDHI MSAADA WA BOTI KUSAIDIA MAMA WAJAWAZITO NA WAGONJWA MWAMBAO WA ZIWA RUKWA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiwakabidhi funguo ya boti na "Life Jacket 8" kwa Uongozi wa kijiji cha Ilanga/Muze ikiwa ni sehemu ya msaada wa boti na Injini moja kusaidia huduma za afya ya mama wajawazito na wagonjwa mwambao wa Ziwa Rukwa. Msaada huo wenye thamani ya Shilingi Milioni 20 umetolewa na Mfadhili Bi. Adrianne Strong kwa kushirikiana na waumini wenzake wa Kanisa la University United Methodist Church la Washington DC Marekani, Mfadhili huyo alishawishika kutafuta msaada huo baada ya kufika Mkoani Rukwa katika kufanya utafiti na kubaini mambo mengi ikiwemo umbali kati ya wananchi na vituo vya kutolea huduma za afya.

Hapo awali yalifanyika majaribio ya Boti kabla ya makabidhiano rasmi.
Kabla ya makabidhiano ya Boti hiyo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aliamuru Boti hiyo kupelekwa ziwani kwa ajili ya majaribio.
Haikuwa kazi rahisi kwani Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya aliwaongoza viongozi wengine wa Chama na Serikali ya Mkoa na Halmashauri kuvua viatu na kukanyaga maji ili kuweza kufikia Boti hiyo iliyobebwa na wananchi wa kijiji cha Ilanga hadi ziwani.
Wananchi wa kijiji cha Ilanga wakishirikiana kubeba Boti hiyo hadi ziwani.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiongea na wananchi wa Kijiji cha Ilanga muda mfupi kabla ya kukabidhi msaada huo kwa uongozi wa kijiji. Katika hotuba yake hiyo aliwashukuru wote waliosaidia upatikanaji wa msaada huo ambao ni Bi. Adrianne Strong na waumini wenzake wa Kanisa la University United Methodist Church la Washington DC Marekani, Dkt. Francis Mashigala wa Hospitali  Kuu ya Mkoa wa Rukwa aliyekuwa anaratibu msaada huo na Bwana Hussein Kandoro (Mwanasheria Ofisi ya Waziri Mkuu) aliyesaidia kusafirisha Boti hiyo kufika Mkoani Rukwa. Kwa upande mwingine aliuita mwaka huu mpya 2014 kuwa ni mwaka wa afya ambapo alihamasisha juu ya upimaji wa virusi ya Ukimwi, kupiga vita unyanyapaa na Ukimwi, mama wajawazito kujifungulia kwenye vituo vya afya na kupeleka shule watoto wenye umri wa kwenda shule.  
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halamashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Ndugu Adam Misana akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ilanga na kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kuzungumza na wananchi wake. Katika kauli yake alisistizia agizo la Mkuu wa Mkoa wa Rukwa la kuhakikisha kuwa shughuli za uvuvi katika ziwa Rukwa zinafungwa kwa muda wa miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi kupisha mazalio mapya ya Samaki. Alisema kuwa doria zitaendeshwa katika Ziwa hilo na yeyote atakaekamatwa akivua katika kipindi hicho hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. 
Dkt. Francis Mashigala wa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Rukwa aliyekuwa mratibu wa msaada huo wa Boti akitoa maelezo mafupi juu ya msaada huo  kwa wananchi wa kijiji cha Ilanga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na Msafara wake walipata fursa ya kutembelea Shamba darasa la moja ya shule zilizopo katika kata ya Mtowisa kwenye kijiji cha Ilanga ambalo limepandiwa kwa mbolea aina ya Minjingu Mazao. Serikali ya Mkoa ikiongozwa na Injinia Manyanya ilitoa agizo kwa kila shule kuwa na shamba angalao ekari tano zitakazotumika kama shamba darasa na kusimamiwa na Afsa Ugani wa eneo husika na kupatiwa ruzuku ya pembejeo inayotolewa Serikali. 

Mpango huo una faida mbili ambapo licha kuwa shamba darasa pia utatibu tatizo la ukosefu wa chakula mashuleni na hivyo kuongeza mahudhurio na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.  (Na Hamza Temba - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa @Rukwareview.blogspot.com)
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Rukwa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa